Watu wawili wamekufa mkoani Mara katika matukio mawili tofauti.
Akizungumzia matukio hayo Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Audax
Mjaliwa alisema katika Mtaa wa Nyamatare Manispaa ya Musoma, mwalimu
Tengeru Mongu (43) wa Shule ya Msingi Igina wilayani Serengeti alikutwa
amejinyonga katika chumba cha binamu yake Mauma Machunde.
Akisimulia mkasa huo binamu wa marehemu huyo alisema, alipoamka jana
asubuhi, alikwenda kumgongea mgeni wake huyo bila mafanikio hali
iliyomchanganya na kutoa taarifa kwa majirani waliofika kumsaidia
kuvunja mlango.
Machunde alisema, baada ya mlango kuvunjwa alimkuta binamu yake
akining’inia juu ya dari akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka na sababu
za kujinyonga hazijajulikani kwani hakuacha ujumbe wowote.
Mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema, marehemu mwalimu huyo
alipata uhamisho kutoka Serengeti kwenda Wilaya ya Butiama, uhamisho
ambao aliuomba kwa madai kuwa umri alionao anafaa kufanyia kazi maeneo
ya nyumbani kwao.
Katika tukio jingine basi lililosadikiwa kuwa ni la Kampuni ya Peace
Maker katika Barabara ya Bunda - Kiabakari kwenye Kitongoji cha Kibisa,
Kijiji cha Nyamisisi, Butiama limemgonga mtembea kwa miguu jana usiku
saa mbili usiku na kumsababishia kifo cha papo hapo.
Akizungumzia ajali hiyo mtoto wa marehemu, Alfred Kitambara, Veronika
Kitambara alisema, baba yake ni Mtendaji wa Kata ya Kyanyari na
alipopata ajali hiyo alikuwa akitoka katika mkutano wa kijiji akiwa
anaendesha pikipiki.
Kitambara alisema, wakati baba yake akiwa njiani alipata ajali ya
pikipiki ambapo alipiga simu nyumbani na kumweleza mama yake kuwa
amepata ajali ya pikpiki amegonga jiwe akaanguka na kudai kuwa hali yake
siyo nzuri hivyo alimtaka mama kwenda kumsaidia.
“Wakati mama akiwa njiani alikutana na watu wakisema kuwa basi
limemgonga mtu lakini halijasimama sidhani kama mtu huyo atakuwa
amepona, kufika katika eneo la tukio alikuta aliyegongwa ni baba lakini
pikipiki ilikuwa mbali kwa maana hiyo alikuwa ameiacha akawa anatembea
ndiyo akagongwa,” alisema Kitambara mtoto wa marehemu.
Kaimu Kamanda wa Polisi alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba polisi
wanaendelea kuchunguza magari ya kampuni hiyo ili kubaini ni gari lipi
lililogonga kwa madai kuwa hakuna gari iliyofika kituoni kutoa taarifa
hizo.
No comments:
Post a Comment