Tafsiri ni nini? Tafsiri kama Taaluma (somo) Tafsiri kama zao, (kile
kinachopatikana baada ya kutafsiriwa/outcome. Newmark (1982) Tafsiri ni jaribio
la kuwasilisha ujumbe uleule ulioandikwa katika lugha moja kwa lugha nyingine.
Jaribio kwa sababu si mara zote unaweza kufanya hivyo kwani unaweza kushindwa
au kufaulu. * Udhaifu wa Newmark katika fasili yake ni kwamba hakuzingatia umbo
la kazi yenyewe au mtindo wa kazi yenyewe. Mfano; kadi ya mwaliko, barua nk.
Mwansoko na wenzake (2006)
Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (Transferring) wa
mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine. * Ukiangalia
wataalamu hawa wawili utaona kwamba wanafanana; kwani wanaona kuwa tafsiri
hufanywa katika maandishi. Nida na Taber (1969) wanaona kuwa tafsiri hujumuisha
upya ujembe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asilia vya lugha lengwa
vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo. Kwa
mfano; “Damu nzito kuliko maji” – "Blood is thinker than water”. Ndugu
yako ni muhimu zaidi kuliko mtu mwingine. “Ukistaajabu ya Musa utaona ya
Firauni” – “Wonders never end” * Nida na Tiber wanaona kuwa katika tafsiri kitu
muhimu ni kuzingatia maana na mtindo.
MFASIRI NI NANI? Ni mtu yeyote anayejishughulisha na kazi za
kutafsiri. Ni mtu mwenye taaluma au ujuzi wa kutafsiri na ambaye
anajishughulisha na kazi hizo (weledi-Professionalism)
MATINI NI NINI? Ni
wazo au mfululizo wa mawazo ambao unajitosheleza kimaana. Matini inaweza kuwa
neno moja, kirai, kishazi, sentensi, aya, kifungu cha habari nk.
AINA ZA MATINI (Text) Kuna aina mbili za matini ambazo ni
Matini Chanzi/Chasili na Matini Lengwa/matini tafsiri. · Matini Chanzi/chasili
(MC) “Source Text” ni matini ambayo iko katika lugha yake ya awali au lugha
yake iliyoandikiwa kabla ya mchakato wa kutafsiri. · Matini Lengwa/tafsiri (ML)
“Target Text” ni matini iliyotafsiriwa kutoka lugha yake iliyoandikiwa. Lugha
Chanzi/Chasili (LC) ni lugha iliyotumika kuandikia matini chanzi (Source
language) Lugha Lengwa (LL) (Target language) ni lugha iliyotumika kutafsiria
matini chanzi au lugha unayoitumia kufanyia tafsiri. KISAWE/USAWE
(EQUIVALENT/EQUIVALENCY) Katika muktadha wa tafsiri kisawe ni neno, kirai,
kishazi, sentensi au hata maneno katika lugha lengwa ambayo maana na matumizi
yake yanalingana au kukaribiana na yale ya neno, kirai, kishazi, sentensi au
msemo mwingine katika lugha chanzi DHIMA / UMUHIMU WA TAFSIRI · Ni njia ya
mawasiliano/daraja kati ya watu au jamii mbili zinazotumia lugha tofauti.
Mfano; maelezo mbalimbali ya jinsi ya kutumia bidhaa mbalimbali kama vile
redio, simu, kurunzi, dawa, jokofu nk. · Ni nyenzo ya kuelezea utamaduni kutoka
jamii moja kwenda jamii nyingine. Mfano; kupitia dini – tafsiri ya Biblia au Kuruani
“Koran”, Pia hata katika burudani – tafsiri ya vitabu mbalimbali ambavyo vina
vipengele vingi sana vya utamaduni kama vile nyimbo nk. · Ni mbinu ya
kujifunzia au kufundishia lugha kimsamiati na kisarufi. · Ni kazi ya ajira kama
kazi nyingine, hivyo huweza kumpatia mtu kipato. · Humliwaza mfasiri; hii ni
baada ya kumaliza kufasiri. SIFA ZA MFASIRI BORA. · Awe mahiri wa lugha mbili
zinazohusika; kuwa mahiri katika lugha maana yake nini? Ni kujua vizuri nyanja
mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile; Fonolojia-Matamshi,
Mofolojia-Maumbo, Sintaksia-Muundo na Semantiki-Maana. · Ajue vizuri utamaduni
wa watu mbalimbali. · Ajue angalau lugha mbili · Awe na maarifa ya TEHAMA (ICT)
· Awafahamu watu, jamii na utamaduni wao – mitazamo kuhusu watu, mitazamo –
kuhusu wanyama. · Apende kujisomea na kujiendeleza kulingana na mabadiliko ya
jamii. Mfano; kusoma vitabu, majarida, magazeti mbalimbali kusikiliza redio na
kuangalia TV nk. · Awe mwandishi bora. MAADILI YA MFASIRI BORA (ETHICS) · Awe
mwaminifu kwa matini na kwa mwenye matini; yaani asipotoshe habari au kusema
uongo. · Awe mchapakazi (Kujituma/Bidii katika kazi) · Awe nadhifu –
Unadhifu-mwonekano wa moyo, asiwe tapeli/laghai · Aelewe/kuelewa taratibu za
kazi na kuzifuata. Mfano; bei ya kutafsiri kwa ukurasa au kwa maneno. ·
Ushirikiano/kushirikiana na watu mbalimbali wa fani mbalimbali, makundi
mbalimbali ikiwa pamoja na wafasiri wenzake. NADHARIA YA TAFSIRI Maana; ni
maelezo muhimu kuhusu vipengele mbalimbali vya kifasiri ambavyo vinapaswa
kufuatwa au kuzingatiwa na kila mfasiri pindi anapokabiliwa na kazi ya
kufasiri. Nadharia ya tafsiri ndio nguzo au mhimili muhimu wa shughuli zote za
tafsiri. Vipengele vingine vitakavyojadiliwa katika nadharia ya tafsiri ni
pamoja na taaluma zinazohusiana na tafsiri na dhima ya nadharia ya tafsiri.
Sababu za kuanzishwa kwa nadharia za tafsiri. Newmark (1982), Mwansoko na
wenzake (2006) wanasema kuna mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa
nadharia ya tafsiri ambayo ni:- i) Wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa
awali; ilionekana kwamba, kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya
kimuundo, kimaumbo, kimsamiati nk. Pia ilikuwa ni nadra/muhali kupata tafsiri
zisizokuwa na makosa. ii) Kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya asasi
zinazojishughulisha na kazi za tafsiri. Hali hii ilisababisha kubuniwa kwa
nadharia ya tafsiri ili kuwepo kwa misingi inayokubalika. Mfano; nchini
Tanzania peke yake kuna asasi nyingi zinazojishughulisha na tafsiri kama vile:
BAKITA, TATAKI, SHIHATA, WAFASIRI na vyombo mbalimbali vya habari kwa mfano:
TV, Magazeti nk. iii) Mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hasa
Sayansi na Teknolojia. Hivyo nadharia ya tafsiri ilianzishwa kwa lengo la
kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili kuwe na
ufanisi zaidi.
TAALUMA NYINGINE
ZINAZOHUSIANA NA TAFSIRI
Tafsiri inauhusiano
mkubwa na taaluma nyingine au vipengele vingine kama ifuatavyo: Inauhusiano na
isimulinganishi; Isimulinganishi hijishughulisha na kulinganisha vipengele
mbalimbali vya kiisimu vya lugha mbili au zaidi, pamoja na kuchunguza mbinu za
ulinganishi huu. Uhusianao wake na tafsiri;- humsaidia mfasiri kuelewa mifumo
ya lugha mbalimbali na jinsi luhga hizo zinavyotumia vipengele vyake vya
kiisimu kutolea taarifa mbalimbali. Inahusiana na isimujamii;- Isimujamii
inahusika na kuchunguza uhusiano kati ya lugha fulani na jamii ambayo inatumia
lugha hiyo. Rejesta mbalimbali za kijamii pamoja na maingiliano baina ya lugha.
Ujuzi wa isimujamii unamsaidia mfasiri kufahamu athari zinazotokana na mahusiano
baina ya lugha na jamii husika na kuzingatia mambo mbalimbali katika kutafsiri.
Inauhusiano na semantiki/pragmatiki;- Semantiki ni taaluma inayochunguza maana
ya maneno katika upweke na katika makundi/taaluma inayochunguza maana ya maana.
Kwa kuwa kinachotafsiriwa ni mawazo au maana ya matini (siyo neno pwekepweke)
basi ujuzi huu wa semantiki utamwezesha mfasiri kujua au kung’amua kuwa maana
ya matini hiyo haitokani na maana ya neno mojamoja badala yake inatokana na
maana ya kimatumizi kwa ujumla katika mktadha mahususi. Inauhusiano na
elimumitindo (stylistics);- Hii inahusu uainishaji wa mitindo mbalimbali ya
lugha na miktadha ya matumizi yake. Elimumitindo Mitindo Mazingira ya kutumia
Uhusiano wake na tafsiri;- Taaluma hii ya elimumitindo itamwezesha mfasiri
kubaini mtindo wa matini chanzi ambao haunabudi kuhamishiwa katika matini
lengwa. Inauhusiano na mantiki (logic);- Mantiki inahusu ukweli na uhakika au
usahihi wa mambo kama inavyosemwa, kuandikwa au kuaminika kwa watu. Mantiki
humsaidia mfasiri kubaini kauli zisizo dhahiri na zinazokanganya katika matini
chanzi ili azirekebishe kwanza kabla ya kuanza kutafsiri. Kwa mfano; The
current president of United Republic of Tanzania is Mzee Ally Hassan Mwinyi. Je
ni kweli?
NADHARIA YA TAFSIRI Nadharia ya tafsiri hushughulikia mambo
makubwa manne ambayo ndiyo dhima ya nadharia ya tafsiri. 1. Kubaini na kufasili
(define) tatizo la kifasiri yaani kazi au mlolongo wa shughuli za tafsiri
zinazopaswa kufanywa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri lililobainishwa. 2. Kuonesha
vipengele vyote vinavyopaswa kuzingatiwa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri
lililobainishwa. 3. Kuorodhesha taratibu au njia zote zinazowezekana
kufanikisha tafsiri inayohusika. 4. Kupendekeza taratibu zinazofaa zaidi katika
kutekeleza zoezi la kufasiri pamoja na mbinu za kutafsiri zilizomuafaka zaidi
kwa matini inayohusika.
NADHARIA MAHUSUSI ZA TAFSIRI.
1.
Nadharia ya Usawe wa Kimuundo;
nadharia hii inatetewa na mtaalam Catford (1969), Tunapofanya kazi ya kutafsiri
tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini
lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini
lengwa. katika nadharia hii muundo ni muhimu. Pia nadharia hii hutumika zaidi
katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia. 2. Nadharia ya Usawe wa
Kidhima; wa tetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida (1964) na Nida na Taber
(1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo.
Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari
zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga
watoto inapaswa iandikwe kiasi kwamba watoto wataweza kuelewa. Pia kwa
kuzingatia nadharia hii unapaswa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na watu
wote. Vilevile tafsiri yako iwe nzuri kiasi kwamba mtu atakaposoma asiweze
kujua kwamba hii kazi imetafsiriwa. 3. Nadharia ya Usawe wa Aina-matini; matini
yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana kwamba kazi
itakayotokea itafanana na matini chanzi. Kma matini chanzi ni ya kisheria
itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Katika
nadharia hii kinachozingatiwa ni fani (muundo) na maudhui (dhima/lengo) ya
matini yenyewe inayotafsiriwa. Watetezi wa nadharia hii ni Reiss (1971), Buhler
(1965) na Newmark (1982/88) 4. Nadharia Changamani (Cross Fertilization
theory). Hii ni nadharia tete iliyoasisiwa na P.S.Malangwa (2010) Ndharia hii
inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu
hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.
UAINISHAJI WA MTINI
Maana: Kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini
katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake.
Sababu: Tunaainisha matini kwa sababu kila matini inahitaji mbinu maalum ya
kuitafsiri. Mikabala/vigezo vya uainishaji: Wataalam wengi wanatumia vigezo
vitatu ambavyo ni Kigezo cha Mada (Topic/Field), Kigezo cha Matumizi ya
Istilahi, Kigezo cha Dhima kuu za Lugha 1. Kigezo cha Mada: katika kigezo hiki
tunaangalia maudhui ya jumla ya matini. Tunajiuliza matini hii inahusu uwanja
gani hasa katika maisha? Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za
matini. i) Matini za Kifasihi (Literary Text); hizi ni matini ambazo zinahusu
fani mbalimbali za fasihi kama vile riwaya, tamthilia, ushairi nk. ii) Matini
za Kiasasi (Institutional Texts); matini hizi ni mtini za kimamlaka kama vile
matini za kisiasa na kiserikali (hotuba, risala, mikataba, vyeti nk). iii)
Matini za Kisayansi (Scientific Texts); matini hizi hujumuisha masuala yote ya
Sayansi na Teknolojia. Kwa mfano; Fizikia, Kemia, Biolojia nk. 2. Kigezo cha
matumizi ya Istilahi: katika kigezo hiki kinachozingatiwa hapa ni kwamba,
matini huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi-msamiati wa uwanja
maalum/husika mf: sharia nk. Kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina tatu za matini:
a) Matini za kiufundi (Technical Text), matini hizi huwa na idadi kubwa ya
istilahi. b) Matini za kinusu ufundi (Semi-Techinical Text), matini hizi huwa
na idadi ndogo au chache za istilahi. c) Matini za zisizo za kiufundi (Non
Techinical Text), matini hizi ni zile ambazo hazina kabisa istilahi bali
hutumia maneno ya kawaida kabisa. 3. Kigezo cha Dhima Kuu za Lugha (Major
Language Functions). Buhler (1965) alipendekeza dhima kuu 3 za lugha. i) Dhima
elezi (Expressive Function), katika dhima hii lugha hutumika kuelezea hisia za
mwandishi/mzungumzaji. Anasema, mzungumzaji au mwandishi hueleza hisia zake
bila kumjali msikilizaji au msomaji. ii) Dhima Arifu (Informative Function),
dhima hii ya lugha hujitokeza pale ambapo matini au lugha inatumika katika kutoa
taarifa kuhusu jambo fulani. Dhima hii huegemea kwenye ukweli wa mambo. iii)
Dhima amili (Persuasive Function) katika dhima hii lugha hutumika kuchochea
hisia za msikilizaji au msomaji. Kiini cha dhima hii ni hadhira. Kwa hiyo, kwa
kuzingatia dhima hizi tatu “3” tunapata aina kuu tatu za matini kama ifuatavyo:
1. Matini Elezi (Expressive Texts); matini hizi huegemea upande wa mwandishi.
Mwandishi hutumia matini hizi kuelezea hisia zake. Mfano, kazi mbalimbali za
kifasihi, hotuba, matini mbalimbali za kimamlaka, matini za kisheria, matini
mbalimbali za kitaaluma, maandishi binafsi nk.
2. Matini Arifu (informative Texts); matini hizi ni zile
ambazo zinatoa taarifa au maarifa kuhusu jambo fulani. Sifa yake ni kuwa
zinakuwa na umbo sanifu au umbo maalum mfano; umbo la jarida, kitabu, ripoti,
tasnifu, vitabu vya taaluma mbalimbali nk.
3. Matini Amili
(Persuasive Texts); matini hizi huegemea upande wa hadhira. Katika matini Amili
mwandishi hujitahidi kadiri awezavyo kuchochea hisia za wasomaji na kuwafanya
watende kama ambavyo mwandishi anataka watende. Hivyo huegemea upande wa
msomaji. Mfano wa matini hizo ni kama vile mialiko mbalimbali, matangazo,
maelekezo mbalimbali nk.
UCHAMBUZI WA MATINI ZA TAFSIRI
Awali ya yote mchambuzi wa matini za tafsiri/mfasiri anapaswa
kusoma matini kwa kina na kuyaelewa kabla ya kuanza zoezi zima la uchambuzi wa
matini. Maana: Uchambuzi wa matini unatuwezesha kubaini sifa na vipengele
vinavyojenga matini husika kimuundo, kidhima na kiitikadi. Hatua/vipengele vya
uchambuzi wa matini: Uchambuzi wa matini unahatua tatu “3” ambazo ni kama
ifuatavyo:
1. Kusoma matini yote na kuielewa vizuri. Hii humsaidia
mfasiri kuweza kuandaa marejeleo muafaka, kuandaa vitabu au machapisho
mbalimbali yatayomsaidia katika zoezi zima la kufasiri matini. Kwa mfano; -
Kuandaa kamusi mbalimbali kama vile kamusi ya lugha chanzi, kamusi ya lugha
lengwa, kamusi ya visawe, kamusi ya fani maalum. - Inamsaidia mfasiri kuandaa
orodha ya istilahi. - Inamsaidia mfasiri kuweza kugawana sehemu au vipengele
vya matini kwa wafasiri wengine.
2. Kuchambua matini yenyewe. Uchambuzi wa matini hulenga
kupata nduni bainifu za matini husika (Distinctive Features). Kipengele hiki
cha pili kina hatua ndogo ndogo tano ambazo ni kama ifuatavyo: a) Kubaini lengo
la mwandishi wa matini chanzi. Mfano; malengo ya mwandishi huweza kuwa kukweza,
kusifu, kukashfu au kuarifu jambo. Kwa kawaida waandishi wa matini chanzi
wanakuwa na mitazamo mitatu; i) Mtazamo hasi kwa mtendwa (biased) mfano, katika
gazeti; “Chelsea yaichabanga Arsenal tatu nunge” ii)Mtazamo chanya kwa mtendwa
(biased) mfano katika gazeti; “Chelsea yafuta uteja kwa Arsenal” iii) Mtazamo
wa kati (neutral) mfano katika gazeti; “Chelsea yaifunga Arsenal au Arsenal
yafungwa na Chelsea” b) Kubaini lengo la mfasiri. Mfasiri anapaswa kujiuliza
kwa nini nafasiri kazi hii? Je lengo langu na mimi ni tofauti na la mwandishi?
- Aepuke upendeleo kwa hadhira chanzi na hadhira lengwa badala yake ajikite
katika ukweli. Hivyo inafaa awe katika mtazamo wa kati (neutral) - Kama kuna
haja ya kuegemea upande mmoja basi aegemee kwa hadhira lengwa. c) Kubaini
hadhira na umbo la matini. Kwa mfano; kama matini chanzi ni kitabu basi matini
lengwa nayo iwe kitabu. d) Kubaini mtindo wa matini. Hapa mfasiri ahakikishe
kwamba mtindo wa matini chanzi unajitokeza katika matini lengwa. Mfano; kama
kuna monolojia au dayalojia basi na matini lengwa inapaswa kuwa hivyo. e)
Kubaini ubora na mamlaka ya matini chanzi. Hapa mfasiri hanabudi kuzingatia
ujuzi wa mwandishi katika kutumia zana za kiisimu/vipengele mbalimbali vya
lugha. Mamlaka hutokana na hadhi au ubobevu wa mwandishi huyo katika taaluma au
fani aliyoandikia. Mfano, kazi ya fasihi ya S. Robert ni bora kuliko
iliyoandikwa na mimi kwa sababu yeye ni mbobevu/galacha katika taaluma hiyo.
3. Kusoma matini kwa
mara ya mwisho. Katika hatua hii ya tatu mfasiri asome tena matini chanzi ili
kutoa taashira (highlight) kuhusu maneno au mambo muhimu. Mambo muhimu ni:
Majina mahususi ya watu, mahali, sehemu au miaka, maeneo ambayo hayatafsiriki
kirahisi ili aweze kuyashughulikia upya hapo baadaye.
MCHAKATO WA KUTAFSIRI/KUFASIRI
Hatua muhimu katika kutafsiri Tunapofanya tafsiri kuna hatua
muhimu kuu sita kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006). Hatua hizo ni kama
ifuatavyo:
1. Hatua ya maandalizi. Hatua hii inahusisha mambo matatu
ambayo ni: a) Kupitia tena sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi,
majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika
kirahisi. b) Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki c) Kutafuta
na kuandika visawe hivyo.
2. Hatua ya pili baada ya maandalizi ni uhawilishaji
(transferring/transference). Katika hatua hii mfasiri uhawilisha ile taarifa
kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa
kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new car is
broken”-langu jipya gari ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili sanifu inapaswa kuwa
“Gari langu jipya limeharibika” Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana,
ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya
lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk. Mbinu ya
tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno
kwa neno.
3. Hatua ya tatu ni
kusawidi rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha
chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya
tafsiri. Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo
haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima
ipitiwe tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).
4. Hatua ya nne ni
kudurusu rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya
kwanza ya kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya
kudurusu haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984)
anasema rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja. Udurusu
unahusisha shughuli zifuatazo: · Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo
isiyoeleweka vizuri. · kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye
matumizi potofu ya visawe. Mfano; “He rarely visits me these days – Siku hizi
ni aghalabu-nadra sana yeye kunitembelea.” ·Kurekebisha sehemu zenye muunganiko
tenge/mbaya ambazo zinazuia mtiririko mzuri wa matini. ·Kuhakiki usahihi na
kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa. Hapa tunaangalia
kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au yamepotoshwa/kubadilishwa.
·Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa kuzingatia
umbo na mada ya matini chanzi. ·Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini
chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.
5. Hatua ya tano ni
kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa
mfasiri au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri anaweza kuwa mteja
wa tafsiri husika au mtu mwingine yeyote unayemwamini. Namna ya kumpa mtu
akusomee rasimu: · Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri · Unampa matini
chanzi na matini lengwa ili alinganishe. Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome
kwa sauti ili uweze kubaini mapungufu. 6. Hatua ya sita ni kusawidi rasimu ya
mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo ya msomaji
ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni ya mteja hutupelekea
kupata rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira, wachapaji nk.
MBINU ZA UUNDAJI WA ISTILAHI
Misingi ya kimataifa ya uundaji wa
istilahi
I.
Istilahi ziwe fupi iwezekanavyo ili zieleweke
vizuri au kirahisi.
II.
Istilahi zifuate sarufi ya lugha lengwa
III.
Tuepuke istilahi za vifupisho/Akronimu
IV.
Tusiunde istilahi kwa kupanua maana
ya istilahi iliyopo.
V.
Istilahi zisiwe na sinonimia au homonimia. -
Kusiwe na maneno kadhaa ambayo yote yanarejelea kitu kimoja. - Au zenye maana
inayokaribiana-homonimia
VI.
Istilahi ziweze kuambatanishwa kuwe na
uwezekano wa kupata istilahi mbalimbali ndani ya kikoa kimoja, mfano;
rekodi-rekodiwa nk. I. Misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili Katika lugha
ya Kiswahili kuna misingi kadhaa ya uundaji wa istilahi za Kiswahili kama
ifuatavyo. i) Istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazolengwa. Mfano;
Istilahi kama vile kionambali – hapa unapata picha ya kile kinachowasilishwa.
ii) Istilahi ambatani zizingatie mambo yafuatayo: - Idadi ya maneno
yanayounganishwa yasizidi mawili. Mfano; Mwanajeshi. - Kama istilahi hizi ni
maneno mawili usitumie kistari (-) - Zisizidi silabi nane. iii) Istilahi ziweze
kunyambulika ili kuunda istilahi zaidi za vikoa. (semantiki field) mf; soma,
somea, someana, someaneni, someshanani nk. iv) Istilahi ziwetoshelevu/zijitosheleze
(precise) na zisiwe ndefu mno. Pia zijitosheleze kimaana. v) Ziwe fupi na
zinazoeleweka kirahisi. Mfano; Istilahi “Autumn” – majira ya majani kupukutika
karibu na kipupwe. Hii si Istilahi bali ni ufafanuzi wa istilahi “Autumn.” vi)
Istilahi mahuluti (blending – mix & combine), finyazo (acronyms) zafaa
ziepukwe kwa sababu etimolojia yake niauvulivuli/haiku dhahiri au haieleweki
vizuri. vii) Upanuzi wa maana uepukwe kwa sababu huwachanya watumiaji. viii)
Kila dhana iwakilishwe na istilahi moja tu/yaani kusiwe na maneno mbalimbali
yanayorejelea istilahi ileile.
AINA/MBINU/NJIA YA TAFSIRI/KUFASIRI
Waandishi wengi wanakubaliana kwamba kuna njia nne
zitumikazo katika tafsiri: 1. Tafsiri ya neno kwa neno (word to word
translation) 2. Tafsiri sisisi (literal translation) 3. Tafsiri ya kisemantiki
(semantic translation) 4. Tafsiri ya kimawasiliano I.
I.
TAFSIRI YA NENO KWA NENO/NENO BAADA
YA NENO.
Tunapotafsiri matini kwa mbinu ya neno kwa neno, hapo
tunafanya tafsiri ya matini chanzi kwa kuzingatia maana za msingi za maneno
katika lugha chanzi na kutafuta maneno hayo katika lugha lengwa. -
Tunapotafsiri matini kwa mbinu ya neno kwa neno matini lengwa hufuata sarufi ya
lugha chanzi. (MC – Sarufi LC) - Tunapotafsiri kwa kutumia mbinu ya neno kwa
neno tafsiri yetu huandikwa chini ya neno husika katika kila mstari. Mfano;
Wa/toto/wa/dogo/wa/na/imba/kwa/ furaha Plural/child/ plural/small/they/tens
pre.cont'/sing/by,for/happiness I/like/banana/s/more/than/orange/s
Mimi/penda,kama/ndizi/wingi/zaidi/kuliko/chungwa/wingi
II.
TAFSIRI SISISI Katika tafsiri sisisi
maneno hutafsiriwa pwekepweke kwa kuzingatia maana zake za msingi katika lugha
chanzi. Tafsiri sisisi huzingatia sarufi ya lugha lengwa. Mfano; - Walimsaidia
katika mahitaji yake ya msingi - They helped him/her in his/her needs of basic
- Walimpa msukumo mkubwa katika biashara yake. - They gave him/her a big push
in his/her business - One day my dreams will come true - Siku moja ndoto zangu
zitakuja kweli Faida ya mbinu hii: - Husaidia kufasiri dhana au matini
zisizotafsirika kirahisi. Mfano; majina/maandishi ya kanga, misemo, nahau nk.
Dosari za mbinu hii: - Si mbinu nzuri kutafsiri matini ndefu ingawa ni mbinu
bora ikilinganishwa na mbinu ya neno kwa neno.
III.
TAFSIRI YA KISEMANTIKI/WAZI -
Huegemea zaidi upande wa mwandishi au upande wa matini chanzi - Hulenga
kufasiri kila kipengele katika matini chanzi. - Huzingatia sarufi ya lugha
lengwa - Huzingatia zaidi maana ya matini chanzi kiasi kwamba huwa na mwelekeo
wa kuwa fafanuzi kwa sababu inataka kufasiri kila kipengele kilicho kwenye
matini chanzi. Kwa mfano; o Tanzania Electric Supply Company Limited o Kampuni
tanzu ya usambazaji umeme Tanzania o Alikwenda mpaka nyumbani kwake o She/he
went up to her/his home o Wonders never end o Maajabu kamwe hayaishi Faida ya
mbinu hii: - - Husaidia sana kufasiri matini elezi - Husaidia kuitajirisha
lugha lengwa kwa misemo au semi mbalimbali. Kwa mfano; Natambua uwepo wako (I
acknowledge your presence) Haijalishi (It doesn’t matter) Mwisho wa siku (At
end of the day) Mwisho lakini si kwa umuhimu (Last but not least) Hasara ya
mbinu hii: - Hukosa vionjo na kumfikirisha sana msomaji - Mbinu hii huwa ni ya
mzunguko na ya kifafanuzi mno. Mfano; Tafsiri ya neno Autumn IV.
IV.
FAFSIRI YA MAWASILIANO/KIMAWASILIANO AU
TAFSIRI HURU - Mbinu hii huegemea zaidi upande wa hadhira lengwa - Huzingatia
utamaduni, itikadi, mazingira na historia ya jamii lengwa. - Hulenga msomaji wa
matini lengwa apate athari ileile kama waipatayo wasomaji wa matini chanzi. -
hii ndiyo mbinu ya tafsiri inayotumika kutafsiria matini nyingi zaidi kuliko
mbinu zilizotangulia na kwa sababu hii ndiyo mbinu bora zaidi ya nyingine mbinu
hii hufaa zaidi kufasiria matini Arifu na Amili. - Katika mbinu hii mfasiri
hutafuta visawe katika lugha lengwa kama vile misemo na methali ambazo maana
zake na muktadha wake wa matumizi hufanana na methali au misemo ya lugha chanzi
au matini chanzi. Kwa mfano; a) Walimpa msukumo mkubwa katika biashara yake
They gave him a big support in his business They helped him a lot in his great deal/in
his business b) Tanzania Electric Supply Company Limited Shirika la Umeme
Tanzania c) Wonder never end Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni
TAFSIRI NA UKALIMANI
Ukalimani
ni nini? Ukalimani ni uhawalishaji wa taarifa au ujumbe kutoka kwa msemaji wa lugha
chanzi kwenda katika lugha lengwa kawa njia ya mdomo au mazingumzo. Katika
ukalimani matini chanzi huwa katika mazungumzo na matini lengwa pia huwa katika
mazungumzo. Katika ukalimani mkalimani hana muda wa kutosha wa kujiandaa kwa
sababu anatakiwa kukalimani kile anachosikia wakati ambapo mzungumzaji
anaendelea kuzungumza mambo mengine. Aina za ukalimani Kuna aina mbalimbali za
ukalimani kutegemeana na vigezo unavyotumia kuainisha au kupata hizo aina; 1.
Kigezo cha kwanza ni kigezo cha Muktadha; Katika kigezo hiki vipengele
vinavyojitokeza ndani ya muktadha ili kupata aina tunazingatia mahali, lengo,
aina ya hadhi, sifa za walengwa nk. Ukalimani wa Kijamii/community
interpretation: Huu ni ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya
kijamii kama vile afya, ujenzi wa shule huduma za kijamii kama vile maji,
umeme, masuala ya mihadhara ya kidini nk. Ukalimani wa Mikutano au
Makongamano/Conference; Huu ni ukalimani unaofanyika katika makongamano au
mikutano mbalimbali. Mara nyingi aina hii ya ukalimani inafanyika katika
mikutano ya kimataifa. Ukalimani wa Mahakama/Mahakamani; Aina hii hufanywa na
wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa ukalimani wa
kisheria. Ukalimani wa Kitabibu; Huu ni ukalimani ambao unafanyika mahali
ambapo matibabu yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina hii ya ukalimani
inafanyika katika hospitali kubwa kubwa. Ukalimani wa Habari/katika vyombo vya
habari; Huu ni ukalimani unaofanywa katika vyombo mbalimbali vya habari,
hususani redio na televisheni ili kuiwezesha hadhira lengwa iweze nayo kuelewa
matangazo yanayotolewa kwa lugha chanzi. Ukalimani Sindikizi/Escort
interpretation; Katika aina hii ya ukalimani mkalimani hufuatana na mtu au
kikundi cha watu katika safari au katika usaili au mahojiano. 2. Kigezo cha pili
ni kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha/Language mode/modality; Katika kigezo
hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya
kusema/kizungumza na lugha ya alama. Kupitia lugha ya alama tunapata aina moja
ya ukalimani yaani ukalimani wa viziwi Kwa kupitia lugha ya mazungumzo au
kusema tunapata aina mbili za ukalimani ambazo ni; Ukalimani
Mfululizo/Andamizi/Simultaneous interpretation; Katika ukalimani mfululizo,
kama jina lenyewe linavyodokeza mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji
wa lugha chanzi. Katika aina hii ya ukalimani mkalimani lazima afanyekazi kwa
haraka sana ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kuepuka kupitwa na mambo
muhimu. Katika ukalimani mfululizo makalimani huketi katika chumba maalum cha
ukalimani (booth) ambacho hakipitishi sauti (sound proof) na kisha huzungumza
kwa kutumia kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa lugha chanzi
kupitia visikizio (ear phones) Ukalimani Fuatishi/Mtawalia (Consecutive
interpretation); Katika ukalimani fuatishi makalimani huzungumza/hukalimani
baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza ujumbe wake au hata kama
hajamaliza ujumbe wake baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde
kadhaa ili kumpa makalimani fursa ya kukalimani kile kilichosemwa. Katika aina
hii mkalimani na mzungumzaji wa lugha chanzi mara nyingi wanakuwa pamoja wakiwa
wamesimama kwenye jukwaa au wakiwa wameketi mezani.
SIFA
ZA MKALIMANI BORA. ·
Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha
anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake. · Ajue lugha zaidi ya mbili za
kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo unavyokuwa mkalimani bora
zaidi. · Awe na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja
unaozungumziwa. Inamaana kwamba kama wewe ni mfasiri wa masuala ya kiuchumi basi
hupaswi kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa
na wanasheria. · Awe na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata
mafunzo ya ukalimani. Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina,
changamoto na namna ya kuzikabili. · Mfasiri anatakiwa awe mchapakazi, mdadisi
na apende kujiendeleza au kupata habari kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii
mfano; magazeti, majarida, televisheni, facebook, twitter au kuzungumza na
watu/kuchangamana na watu. · Awe na kipaji, yaani: Uwezo wa kukumbuka Kuteua
msamiati sahihi kwa haraka Kipaji katika kuunda istilahi haraka haraka na
kuitumia. Kipaji cha ulumbi/awe na ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta
watu (eloquency) · Awe na uzoefu.
UMUHIMU
WA UKALIMANI
1.
Ukalimani ni daraja linalosaidia kuunganisha watu au jamii inayozungumza lugha
tofauti.
2.
Ukalimani ni nyenzo ya kueneza utamaduni. mfano; dini
3.
Ukalimani husaidia katika masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa.
Mfano; usuluhishi wa migogoro.
4.
Ukalimani hutumiwa na makampuni ya simu kuwasiliana na wateja wao
5. Ukalimani husaidia kufanikisha vikao,
mikutano na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Mfano; mikutano ya UN, AU nk.
6.
Ukalimani hutumika kama mbinu ya kijifunzia lugha ya pili au lugha ya kigeni
hasa katika hatua za awali.
7. Ukalimani unamsaidia mkalimani mwenyewe
kujifunza lugha.
STADI
MUHIMU KATIKA UKALIMANI
i)
Lugha na mawasiliano;- kumudu stadi
za lugha na mawasiliano
ii)
Kuwa na stadi ya kusikiliza iii) Stadi ya
kudondoa (kuandika muhtasari) – kuchukua mambo muhimu tu kati ya mengi
anayoongea.
iii)
Stadi ya kumbukumbu/kukumbuka (memory rehesion
skill)
iv)
Sanaa ya kuzungumza hadharani. mfano; jinsi ya
kuandaa hotuba, jinsi ya kuanza kwa kishindo, jinsi ya kumaliza kwa kishindo,
kutoa mifano dhahiri, kuepuka kujisifia, Toa visa vya kweli/mara nyingi
inashauriwa kutoa visa vyako/vinavyokuhusu wewe, kuepuka vitabia vinavyokera
mfano; kuchokonoa puani, kujikuna kuna nk. vi) Hakikisha umevaa vizuri nk.
TAFSIRI NA UKALIMANI: KUFANANA NA KUTOFAUTIANA.
Tofauti kati ya tafsiri na ukalimani: vipengele/vigezo vya
kutofautisha dhana hizi mbili; a) Dhana (maana/fasili) b) Lugha (mtindo, stadi
maalum nk) c) Utendaji (mf; vifaa/zana) d) Kigezo cha
mada/maandalizi/uhawilishaji e) Mfumo wa lugha (kuzungumza au kuandika) f)
Uwasilishaji (mara moja tu au kuna nafasi ya kudurusu) g) Hadhira (papo kwa
papo au mbali) h) Maslahi/malipo (utaratibu wa kutoza pamoja na tozo
lenyewe/bei mf; kwa ukurasa au maandishi/saa. i) Ukongwe/umri/historia (kipi
kilianza) j) Stadi muhimu za lugha zinazohitajika. mfano; kusoma, kuandika,
kusikiliza na kuzungumza.
KUFANANA KWA TAFSIRI NA UKALIMANI
a)
Vigezo b) Njia (kibebeo) c)
Lengo/dhima d) Vijenzi (vipengele vya modeli/muundo wa mawasiliano, mfano;
sender – channel – receiver – feedback. e) Faida
TATHMINI KATIKA TAFSIRI (TRASLATION
CRITICISM)
Katika tafsiri tunafanya tathmini ili kujua
ubora na upungufu wa tafsiri husika. Kutathmini tafsiri ni zoezi la kupima
kiwango cha ubora wa tafsiri husika kwa kutumia mbinu zinazokubalika.
Tunapotathmini tafsiri tunaweza kupata makundi yafuatayo ya tafsiri hizo
tunazotathmini; · Tafsiri bora (good translation) · Tafsiri tenge/mbaya
(mistranslation) · Tafsiri finyu (under translation) · Tafsiri pana (over
translation)
TAFSIRI BORA; hii ni ile tafsiri
ambayo kifani na kimaudhui inaendana na matini chanzi. TAFSIRI TENGE; hii ni
ile tafsiri ambayo haiendani na matini chanzi. TAFSIRI FINYU; hii ni ile
tafsiri ambayo imeacha vitu vingi katika kutafsiri. TAFSIRI PANA; hii ni ile
tafsiri ambayo imeongezwa mambo mengi ambayo hayapo katika matini chanzi au
imefasiriwa kijumla jumla.
AINA
ZA MATINI LENGWA ZINAZOFAA KUTATHMINIWA
Kuna aina mbili za matini lengwa
ambazo zinafaa kutathminiwa kama ifuatavyo: a) Matini lengwa zilizo katika
mchakato wa kufasiriwa, hii ni ile matini ambayo bado haijafikishwa kwa
walengwa. Mfasiri anaweza kutathmini upya matini kabla ya kuifikisha kwa
mlengwa. b) Matini zilizo mikononi mwa mtumiaji/mteja/hadhira. Fursa ya
kuboresha kazi hiyo haipo ila hufanyiwa tathmini ili kutoa maoni ambayo yatamwezesha
mfasiri kuboresha kazi nyingine zinazofuata au toleo linalofuata.
MBINU ZA KUTATHMINI TAFSIRI
1. Ulinganishaji wa matini; hii
ndiyo mbinu kongwe zaidi na ndiyo inayotumiwa na wahakiki wengi zaidi (MC na
ML). Katika mbinu hii kinachofanyika ni kwamba matini lengwa hulinganishwa na
matini chanzi ili kubaini vipengele vya kimuundo na kimtindo vilivyoongezwa,
vilivyopunguzwa au vilivyopotoshwa ili kuvifanyia marekebisho. 2. Kupima
uasili; tafsiri bora haipaswi kusomeka kama tafsiri. Hii ina maana kwamba mtu
anaposoma tafsiri yako asijue kama ni kazi iliyotafsiriwa badala yake inatakiwa
isomeke kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo. Hali ambapo tafsiri
husomeka kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo ndio ambayo huitwa
uasili. Hapa mfasiri mwenyewe au mtu mwingi anaisoma kazi hiyo. Inashauriwa
apewe mtu mwingine tena bila kuambiwa kwamba kazi hiyo ni tafsiri.
3. Kupima uelewekaji; Katika mbinu
hii kinachoangaliwa ni kueleweka kwa maudhui yanayotolewa katika tafsiri hiyo.
Mtu anayepima uelewekaji atajiuliza yeye mwenyewe, je maudhui katika kazi hii
yataeleweka kwa wasomaji au kazi hii inazungumzia nini? Hivyo inashauriwa
kwamba mfasiri ampe mtu mwingine ili kuepuka kujipendelea. Tahadhari: Mtu
anayepelekewa kazi hiyo inashauriwa awe mfasiri.
4. Kupima usomekaji; Katika mbinu
hii ya kupima usomekaji mfasiri au mhakiki atapima tafsiri husika ili kuona
iwapo inasikika vizuri masikioni mwa msikilizaji na kama inamtiririko
unaokubalika katika lugha lengwa. Hapa kunakuwa na watu wawili mmoja
anasikiliza na mwingine anasoma kwa sauti.
5. Kupima ulinganifu; Katika hii
mhakiki anaangalia umakini wa mfasiri katika kutumia kwa namna inayofaa
vipengele muhimu vya matini kama vile msamiati, istilahi, maudhui au maneno
muhimu yanayobeba maudhui. Maana yake ni kwamba kama neno limejirudia rudia
katika tafsiri usibadilishe, mfano: Aim – nia, lengo, madhumuni, kusudi, azma,
shabaha, kusudi nk. Hivyo kama neno “Aim” umelifasiri kama lengo basi popote
litakapojitokeza kwa mara nyingine katika matini basi libaki hivyohivyo bila
kubadili badili. 6. Tafsiri rejeshi (Back Translation); Ni mchakato wa
kutafsiri matini ambayo tayari imetafsiriwa katika lugha fulani yaani lugha
lengwa na kuirejesha tena katika lugha chanzi kwa lengo la kuitathmini tafsiri
hiyo.
MAREJEO:
Cartford, J. C. (1965). A Linguistic
Theory of Translation. London: OUP.
Larson, L. M. (1984). Meaning-based
Translation. London: University Press of America. Mwansoko, H. J. M. na wenzake
(2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982). Approaches to Translation. Oxford: Pergamon Press. Newmark,
P. (1988). A Textbook of Translation. London: Prentice Hall.
Nida, E. A. (1964). Towards a
Science of Translation. Leiden: E. J. Brill. Nida, E. A. and C. R. Taber,
(1969). The Theory and Practice of Translation. London. Prentice Hall.
No comments:
Post a Comment