Rafiki,
wanawake wengi hulia na kujutia kuwepo katika ndoa, hii ni kutokana na
kuhisi au kujua kuwepo kwa usaliti kwa waume zao. Ukweli ni kwamba suala
la kusalitiwa linaumiza sana, hakuna atakayekuwa tayari kukubali
usaliti katika penzi lake.
Huo
ndiyo ukweli, lakini pamoja na ukweli huo umewahi kujiuliza kwa nini
mpenzi wako anakusaliti? Umewahi kufikiri kwamba hata wewe unaweza kuwa
chanzo cha mpenzi wako kukusaliti?
Kama
hujawahi kufikiri basi fahamu kwamba kama usipokuwa makini katika
maeneo fulani katika ndoa yako, unaweza kuwa chanzo cha mumeo
kukusaliti. Vipengele vifuatavyo, vinafafanua hilo kwa undani zaidi:
UNATAMBUA MAJUKUMU YAKO?
Hili linawashinda wengi katika maisha ya ndoa na waume zao kwa kukosa
kujitambua kuwa yeye ni nani na wajibu wake katika ndoa yake ni upi.
Hapo awali kabla ya kuingia katika ndoa na mumeo ulikuwa ukimnyenyekea
na kujitahidi kadiri ya uwezo wako kumwonyesha mapenzi motomoto lakini
sasa baada ya kuingia katika ndoa umebadilika.
Ulikuwa
msafi mwenye kumjali wakati wote na kumwonyesha kuwa yeye ni muhimu
maishani mwako na wewe ni muhimu sana katika maisha yake. Kuwa naye
karibu wakati wote na kumshauri hasa akiwa katika matatizo na sononeko
la moyo au msongo wa mawazo vilimvutia na kuona thamani yako kwenye
maisha yake.
Huenda
hapo awali ulikuwa mshauri wake mkubwa wa mambo mbalimbali ya kikazi na
wakati mwingine mambo yake binafsi, wakati alipokuwa na majaribu ya
kufukuzwa kazi au kupata balaa la madeni kazini kutokana na uharibifu au
upotevu wa mali ya anapofanyia kazi kwa kumshauri au hata kumsaidia
kifedha.
Sababu
hizo na zingine nyingi ulizokuwa ukimfanyia wakati mkiwa wachumba
huenda ndizo zilizomsukuma akusogeze karibu ili aishi na wewe kwa
kutambua umuhimu wako katika maisha yake lakini sasa umebadilika!
Mwanaume anahitaji mwanamke wa kumshauri na kumpa moyo hasa anapokuwa kwenye majaribu na matatizo mbalimbali ya kimaisha.
Kama
awali ulikuwa ukimfanyia hivyo mumeo na sasa umeacha ni wazi kwamba
atakapokuwa na msongo wa mawazo au matatizo flani atakwenda baa ambako
atakutana na mwanamke wa nje na akithubutu kumweleza yaliyomsibu atapata
tulizo kwa sababu wanawake wa nje ni mahodari wa kufariji waume za
watu.
Baadhi
ya wanawake wakishaingia katika ndoa, hujisahau na kuona kuwa wao ni
wao na kama walichotaka wameshakipata hivyo kujisahau na kutowapa
wapenzi wao mapenzi motomoto. Kikubwa unachopaswa kutambua wewe mwanamke
ni kwamba wanaume wanapenda kuona wake zao wanakuwa kwa ajili yao na
kuwafanyia vituko vya mahaba kila wakati.
Kadhalika
hupenda kuona wake zao wanakuwa karibu nao wanapokabiliwa na matatizo
mbalimbali ya kimaisha. Hakika utakaposhidwa kumjali mumeo huona ni
afadhali atafute kitulizo kingine ambapo hata hivyo mara nyingi
hukimbilia baa kutafuta kitulizo cha msongo wa mawazo.
Wengine
hushinda kutwa nzima nyumbani wakihudumia mifugo au wakifanya shughuli
ndogondogo za kila siku kama kufua, kupiga deki na kazi nyingine za mama
wa nyumbani baada ya hapo hubaki na nguo alizoshinda nazo kutwa nzima
hadi mumewe anaporejea kazini humkuta akiwa na nguo hizo chafu huku
akinuka jasho ambapo kwa kiasi kikubwa linamkera mume atakaporudi kutoka
kwenye mihangaiko yake.
Hivi
unafikiri kwa misingi hiyo mumeo ataacha kutoka nje ya ndoa kweli? Kama
unakuwa mchafu wakati wote, humfurahishi, huvutii kama zamani unadhani
atafanya nini kama siyo kukusaliti?
Lazima utambue majukumu yako katika ndoa yako. Majukumu yako hayaishii
kumfulia, kumpasia na kufanya usafi nyumbani pekee! Majukumu yako ni
pamoja na kuhakikisha mumeo anafurahia penzi lako pamoja na kumsaidia
katika matatizo mengine ya kikazi na kiakili. Anza kubadilika sasa kabla
KUACHA KUMJALI MWENZAKE
Wakati
fulani, baadhi ya wanawake wakishapata mtoto/watoto humsahau mwanaume
wake na kuhamishia mapenzi yake kwa mtoto/watoto. Kwamba wanashidwa
kugawanya mapenzi vyema kati ya mumewe na mwanawe.
Hili
limekuwa tatizo kubwa sana kwa sababu baadhi ya wanawake wakishapata
watoto huwasahau kabisa waume zao na kutumia muda mwingi zaidi kuwa na
watoto. Wanawake wa aina hii wapo tayari kulala usiku mzima akiwa
amemgeukia mwanaye na kumpa mgongo mumewe hadi asubuhi.
Kwa
kufanya hivyo wanashidwa kufahamu kuwa mume ataona kuwa hawajali, hivyo
kuchochea hamu ya kutafuta hifadhi nyingine nje ya ndoa. Habari mbaya
kwao ni kwamba, wanawake wa nje huwa wataalamu na wajanja sana katika
suala zima la mapenzi, hivyo kumfanya mwanaume kuwa mpofu dhidi ya mkewe
kutokana na kuzama katika mapenzi mazito ya kiruka njia!
Rafiki
zangu, mnapaswa kutambua kitu kimoja, japokuwa una mtoto tena
anayehitaji mapenzi na huduma zako lakini tambua kuwa una mumeo ambaye
pia anahitaji mapenzi yako. Hakika kilio hiki hakiwezi kuisha kama
wanawake wa aina hii hawatabadilika na kuwajali waume zao.
Tambua
kuwa bila mumeo huyo mtoto wako unayemjali na kushinda naye kutwa nzima
ukimmbembeleza kadhalika usiku kucha akiwa ubavuni mwako asingekuwepo!
Jitahidi kugawanya mapenzi kwa mwanao na mume wako.
Tambua
kuwa wanawake wa nje maarufu kwa jina la vimada ni wajanja sana tena
wenye mbinu nyingi za kuwanasa waume za watu wasifurukute kwa lolote kwa
kuwapa mapenzi motomoto kiasi cha kuweza kusahau nyumba zao.
TABIA YA ASILI?
Baadhi ya wanaume wana hulka mbaya za kupenda kuwa na wanawake tofauti
tofauti kwa minajili ya kuangalia ladha tofauti za mapenzi! Wanaume wa
aina hii wapo, hata wakipewa mapenzi ya aina gani hulka hii mbaya
waliyonayo huwasukuma kuwa na wanawake wengine wa nje.
Wanaume
hawa hupenda kuwa na wanawake tofauti kutokana na tamaa zao za kimwili.
Mwanaume wa aina hii ni rahisi sana kumtambua unapokuwa katika uhusiano
naye kabla ya kuingia katika ndoa.
Mara
nyingi hata unapotoka naye katika matembezi ya jioni au kwenye kumbi za
burudani, huweza kusifia mwanamke mwingine aliyepita karibu yenu.
Mwanaume wa aina hii hashindwi kukueleza anavyovutiwa kimapenzi na
mwanamuziki, mnenguaji au mwigizaji fulani mnapokuwa pamoja katika
matamasha yao au mnapoangalia runinga yenu nyumbani.
Tabia
za mwanaume wa aina hii huonekana mapema na hivyo ukiona alama hizi ni
vyema ukaepukana naye mapema kabla ya kuingia katika ndoa ambayo kwa
hakika itakuwa chungu kwako! Wanaume hawa hata ukiwapa mapenzi kiasi
gani bado hutoka nje kutokana na hulka yake hiyo mbaya.
ZINGATIO LA MWISHO
Usiruhusu usaliti katika penzi lako, usaliti siyo mzuri hata kidogo
katika maisha ya kimapenzi. Unatakiwa kuhakikisha unatumia kila njia
kuhakikisha kwamba kunakuwa hakuna usaliti katika penzi lako.
Kwa
vipengele hivyo hapo juu, ninaamini kuna mengi mapya uliyojifunza,
unachotakiwa kufanya ni kufanya mabadiliko ya dhati katika ndoa yako.
Mahali ambapo unahisi ulikuwa unakosea, anza sasa kufanya mabadiliko na
uwe mpya katika penzi lako.
Uwezo
wa kuruhusu au kukomesha usaliti katika uhusiano wako upo mikononi
mwako. Bila shaka umenielewa na utafanya kitu fulani cha tofauti katika
maisha yako. Rafiki zangu, mapenzi ni sanaa, kila siku unapaswa kuongeza
ujuzi.
Mwisho
wake ni kwamba, utakuwa bora kila siku na suala la maumivu kwako
litabaki kuwa historia. Niseme nini zaidi ya kukushukuru kwa kutumia
muda wako kunisoma? Ahsanteni sana.
hujampoteza mumeo.
No comments:
Post a Comment