KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeomba Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imuombe Rais atoe kibali cha
ajira kwa walimu kukabili uhaba unaoikabili nchi.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza alitoa ushauri huo jana mjini Dodoma
kwenye kikao kati ya wajumbe wa kamati hiyo na viongozi na watendaji wa
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Naibu
Waziri, Selemani Jafo.
Kikao
hicho kilikuwa ni cha kamati kupokea na kujadili taarifa ya tathmini ya
utekelezaji wa mpango wa ofisi hiyo wa utoaji elimu bila malipo katika
kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu ambako suala la uhaba wa walimu
liliibuliwa na wajumbe.
“Walimu
waajiriwe...ni vyema mumuone rais, angalau afungulie kibali cha walimu
pekee...wanafunzi wanaongezeka mara mbili, lakini walimu hakuna,” alisema Rweikiza.
Awali,
akijibu hoja za wajumbe juu ya changamoto ya uhaba wa walimu, hususan
wa Sayansi na Hisabati, Jafo alikiri hali hiyo kuikumba serikali na
kusema ndiyo maana walilenga kutoa ajira 35,000 kabla ya rais
kusimamisha vibali vya ajira kwa watumishi wote.
Hata hivyo, alisema uamuzi wa Rais ni wa nia njema kuwezesha uhakiki wa watumishi hewa.
Alisema katika kauli ya hivi karibuni ya Rais John Magufuli, alisema wakati wowote kibali kitatolewa.
Jafo alisisitiza kuwa kibali kitakapotolewa, kipaumbele itakuwa ni ajira kwa walimu wa Sayansi ya Hisabati.
Akielezea
namna ya kuziba mapengo ya walimu wa masomo hayo, Jafo alisema serikali
itafikiria pia watu wengine wanaoweza kufaa katika kufundisha masomo
hayo wakiwemo walimu wastaafu na wahitimu wa fani nyingine.
No comments:
Post a Comment