WABUNGE
wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi
ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi.
Hatua hiyo imetokana na kile
kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya
Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12,
mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, wabunge wamedai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito
na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya
taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada
ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge
wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wizara 4 zilizokosa Mawaziri
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri,
Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara
hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara
hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli
aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa
atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi,
Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na
Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii,
ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa
mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
Kinana atoboa siri
Mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Arusha,
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alitoa
siri ya wabunge wanne ambao walipigiwa simu za uteuzi wa uwaziri, lakini
walikataa kwa hofu ya kushindwa kwenda na kasi ya Rais Magufuli.
Alisema anachoamini ni kwamba Rais John
Magufuli, atakuwa aliwaeleza baadhi ya wabunge kuhusu nia yake ya
kuwateua katika nafasi hizo, lakini wao wakamwomba asiwape majukumu hayo
kwa kuwa hawana uhakika wa kwenda na kasi anayohitaji katika Serikali
yake.
Kinana alisema kinachojitokeza sasa ni
kama alivyoshauri Rais Magufuli kuwa si vema kwa waziri aliyeteuliwa
kufanya sherehe nyumbani kwake na kuita marafiki kwa kuwa wana mzigo
mzito katika kuwatumikia wananchi.
“Ni vema mawaziri hawa wakafanya maombi
kwa kuwaita au kuwafuata viongozi wa dini kwani wana kazi ngumu
kulingana na nia njema aliyonayo Rais Magufuli katika kupambana na
masuala ya ufisadi.
“… kazi ya kupambana na ufisadi kamwe si
rahisi hadi kushangilia uteuzi, lengo kubwa ni kuwaletea wananchi
maendeleo kupitia ubinafsishaji wa viwanda kutoka kwa watu
waliomilikishwa na kuviua,” alisema Kinana.
Katibu mkuu huyo wa CCM, alisema anaunga
mkono uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi
dunaini, hali ya kuwa wagonjwa hawana dawa.
“Nyingine ni Wiki ya Maji, mnafanya
maadhimisho huku watu hawana maji, Wiki ya Maziwa wakati wafugaji
wamekonda na mifugo imekonda haitoi maziwa, fedha hizo zitumike kwa
mambo mengine,” alisema Kinana.
******SOURCE***** PERUZIBONGO********
No comments:
Post a Comment