Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza leo imesikiliza
kesi ya iliyofunguliwa na familia ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema
mkoa wa Geita marehemu Alphonce Mawazo. Kesi hiyo ilifunguliwa
na baba mdogo wa marehemu, mchungaji Charles Lugiko, huku mlalamikiwa
namba
moja ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
Mawakili wa upande wa jamhuri wamesema mahakamani hapo kuwa kimsingi
hawapingani na hoja ya mwili wa marehemu Mawazo kuagwa jijini Mwanza. Hata
hivyo, upande huo umeendelea kuonesha mashaka waliyo nayo juu ya kuagwa huko.
Akiwasilisha utetezi wa upande wa mlalamikiwa wa kwanza, wakili
wa serikali Emilly Kiria amesema kuwa wanachopinga ni namna na mazingira ya
uagaji wa mwili wa marehemu huyo. Wakili mwwingine wa upande wa jamhuri, Seth
Mkemwa, alisema kuwa mauaji ya kiongozi huyo yalikuwa ya kikatili, hali ambayo
inaweza kuibua hisia kali kwa waombolezaji wakati wa kuagwa kwake.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Salum Mwalimu akiongea na waandishi wa habari kuhusu kesi ya kuzuiwa kuuaga mwili wa marehemu Mawazo |
Mawakili wa upande wa mlalamikaji, James Ole Milya, John
Malya na Paul Kipeja waliwasilisha mahakamani hapo maombi ya msingi matatu,
wakiiomba mahakama hiyo kutengua amri ya kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza ya
kuzuia kuagwa kwa marehemu Mawazo jijini mwanza. Amri hiyo ya mkuu huyo wa
polisi ilitaja sababu za zuio hilo kuwa ni kuchukua tahadhari dhidi ya mlipuko
wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na kuwepo kwa taarifa za kiintelijensia
kuwa kuna tishio la hali ya usalama jijini humo.
Ombi jingine lililowasilishwa na mawakili hao wa mlalamikaji
ni kuiomba mahakama itoe agizo kuwa amri hiyo ya kamanda wa polisi wa mkoa wa
Mwanza ni batili kisheria, kwani tangazo linalohusiha mlipuko wa magonjwa kama
kipindupindu lilipaswa kutolewa na afisa anayetajwa kisheria na linapaswa
kutolewa katika gazeti la serikali au katika gazeti lisilo la serikali lenye mzunguko
mkubwa katika jamii, na si kamanda wa polisi.
Ombi la tatu lililowasilishwa na mawakili hao ni kuiomba
mahakama hiyo itoe agizo la kumkataka kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza
asijihusishe au asiingilie shughuli za msiba na kuagwa kwa mwili wa marehemu
Mawazo.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Lameck Mlacha imeahirishwa hadi
kesho saa saba mchana ambapo mahakama itakaa kwa ajili ya uamuzi wa kesi hiyo
ya msingi.
Mtoto wa marehemu Mawazo ambaye siku chache zilizopita alifanya mtihani wa darasa la nne huku mwili wa baba yake ukiwa kwenye jokofu la kuhifadhia maiti |
Wakati hayo yakiendelea, mtoto wa kwanza wa marehemu yupo katika mitihani ya taifa ya darasa la nne iliyoanza jana tarehe 25 Novemba na kutarajiwa kumalizika leo. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), watahiniwa wa darasa hilo jana walifanya mitihani ya masomo ya Maarifa ya Jamii, Hisabati, na Lugha ya Kiingereza. Ratiba hiyo inaonesha kuwa leo watahiniwa hao watafanya mitihani ya Sayansi, Kiswahili, Stadi za Kazi, Haiba na Michezo, na Tehama.
Mtoto huyo anafanya mitihani hiyo akiwa katika wakati mgumu huku akifahamu unyama uliotumika kumkata kata baba yake hadi kufa, na pia akifahamu kuwa mpaka sasa mwili wa mzazi wake huyo umehifadhiwa katika jokofu la maiti katika chumba cha kuhifadhia maiti, huku pia kukiwa na mvutano wa kisheria juu ya shughuli ya kuuaga mwili wake.
No comments:
Post a Comment